KESI ya kuua bila kukusudia inayomkabili mtoto mzuri wa Bongo Movies, Elizabeth Michael ‘Lulu’ imewekwa kiporo kufuatia kuwepo kwa kesi nyingi za mauaji mahakamani, Risasi Mchanganyiko limetonywa.
Mtoto mzuri wa Bongo Movies, Elizabeth Michael ‘Lulu’.
Kwa mujibu wa chanzo makini, kuna uwezekano mkubwa wa kesi hiyo kusikilizwa tena Februari mwakani kutokana na mlolongo mkubwa wa kesi za mauaji zilizopo Mahakama Kuu ya Tanzania.
Chanzo hicho ambacho kipo ndani ya kamati ya majaji wanaoshughulikia kesi hiyo, kimenyetisha kuwa kesi ya Lulu itakuwa ngumu kusikilizwa wakati huu kwani mbali na wingi wa kesi mahakamani hapo, lakini pia majaji na mawakili watakwenda likizo.
“Ujue kesi ya Lulu ilikuwa miongoni mwa ambazo zingesomwa kabla ya mwaka huu kuisha, ila kulingana na vikao vya majaji inaonyesha wazi kabisa mwaka huu itakuwa ngumu hata Januari haitawezekana kwani wana kesi kama tatu za mauaji na baada ya hapo watakwenda likizo sambamba na mawakili kwani nao ndiyo kipindi chao cha likizo,” kilisema chanzo chetu.
Lulu anakabiliwa na kesi ya kumuua bila kukusudia aliyekuwa mpenzi wake, Steven Kanumba, Aprili 7, 2012 maeneo ya Vatican-Sinza jijini Dar.Kifo cha Kanumba kilichotokea nyumbani kwake, kilidaiwa kilitokana na kuangukia sehemu ya nyuma ya kichwa ambapo alipata mtikisiko wa ubongo kisha kuzikwa kwenye Makaburi ya Kinondoni, Dar.
No comments