Kiungo wa mpya wa Yanga, Emerson de Oliveira Neves Rouqe akiwa amewasili Dar es Salaam. Picha na Khatimu Naheka
INGAWA baadhi ya wanachama wanakomaa kwamba Mbrazili mpya wa Yanga, Emerson Roque, asisajiliwe mpaka watakapojiridhisha na uwezo wake, Kamati ya Usajili imetamka kwamba kiungo huyo yupo kwenye ubora wake.
Viongozi hao wamejiridhisha kwamba mchezaji huyo atakuwa na manufaa baada ya kuangalia video zake ambapo mmoja wao amemfananisha na kiungo wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Athuman Idd Chuji wakati alipokuwa kwenye ubora wake enzi za nyuma.
Emerson aliwasili nchini juzi Jumatano akiwa na kocha wake, Marcio Maximo, ambaye pia anaamini kwamba atafanya vizuri endapo uongozi wa Yanga utajiridhisha katika majaribio yake yatakayomfanya apewe mkataba.
Kigogo mmoja mwenye ushawishi mkubwa kwenye usajili wa Yanga, aliliambia Mwanaspoti kuwa wameona video mbalimbali za mchezaji huyo akiwa na timu alizowahi kuzichezea nchini humo na kutamka kwamba wamepata kiungo mahiri anayestahili kupewa mkataba kuziba nafasi ya Genilson Santos ‘Jaja’.
Jana Alhamisi asubuhi Emerson katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Loyola alifanya mazoezi na wenzake, lakini Maximo alimpa mazoezi mepesi ya kukimbia akiwa na Andrey Coutinho ambao walichelewa kuanza mazoezi ya pamoja na wenzao walioanza Jumatatu.
“Emerson ana nafasi kubwa ya kusajiliwa kwani tumeona video za mechi zake alizocheza, ni mchezaji mzuri kama alivyokuwa Chuji enzi za ubora wake, kama ataweza kuendana na mfumo wa ligi yetu pamoja na viwanja basi tutakuwa tumepata mbadala wa Chuji au Domayo,” alisema kiongozi huyo mwenye rekodi za aina yake kwenye uongozi wa Yanga ingawa hapendi kutajwa kwenye vyombo vya habari.
“Sisi hatuangalii mchezaji ametoka wapi, tunachojali ni kiwango cha mchezaji husika na kama kocha amemkubali.”
Kuhusu usajili wa wachezaji wengine aliowapendekeza Maximo, alisema kuwa jana Alhamisi jioni viongozi wa Yanga walitarajia kukutana na kocha huyo ili kujadili mambo mbalimbali ya timu ikiwa ni pamoja na utekelezaji usajili wa wachezaji wa ndani ambao ni viungo Jabir Aziz wa JKT Ruvu na Sabri Makame wa Mgambo Shooting.
“Kocha hajazuia wachezaji kuja kufanya majaribio, ametoa uhuru kwamba kama kuna kiongozi ameona mchezaji mzuri amlete ili ajaribiwe, hivyo hata hao wachezaji wengine wa kigeni kama watakuja hakuna tatizo, watajaribiwa ila nani atakatwa itajulikana baadaye kwani Kiiza (Hamis) hawezi kuachwa ameonyesha kiwango kizuri ila hakujapata nafasi tu,” alisema.
Wachezaji wengine wa kigeni wanaotajwa kuja kufanya majaribio Yanga ni Jonas Sakuwaha kutoka TP Mazembe (Jamhuri ya Congo), Yunus Sentemu kutoka AS Vital (Burundi) na Mohamed Traorre wa El Mereikh (Sudan) ambaye anatajwa kupewa mkataba moja kwa moja bila majaribio.
Mpaka sasa Yanga ina nafasi moja ya kujaza katika wachezaji wa kigeni kwani tayari inao wanne; Kiiza, Coutinho, Mbuyu Twite na Haruna Niyonzima. Yanga inaamini kwamba Emerson ana uwezo wa kukaba kwa nguvu pamoja na kutoa pasi za mabao akiziba pia nafasi ya Domayo aliyetimkia Azam FC.
Wakati hilo likiendelea, Maximo ameliambia Mwanaspoti kuwa katika kutaka kukipima kikosi chake kinachojiandaa na mechi dhidi ya Simba ya Nani Mtani Jembe ya Desemba 13, anataka kupata mechi mbili ngumu za kimataifa.
“Nilishawapa kazi hiyo viongozi, ningependa kutafutiwa mechi zitakazotupatia kipimo kabla ya kucheza na Simba. Desemba 13,”alisema Maximo.
No comments